Mkutano wa majadiliano ya wadau kuhusiana na “Umuhimu wa Wadau katika Kuendeleza Ujuzi kwenye Maeneo ya Kazi kupitia Uanagenzi, Mafunzo ya Kazi kwa Wahitimu pamoja na Mafunzo kwa Vitendo”
Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) siku ya Alhamisi tarehe 22 Juni 2023, kilifanya Mkutano wake Mkuu wa 64 ambao ulioambatana na majadiliano ya wadau kuhusiana na “Umuhimu wa Wadau katika Kuendeleza Ujuzi kwenye Maeneo ya Kazi kupitia Uanagenzi, Mafunzo ya Kazi kwa Wahitimu pamoja na Mafunzo kwa Vitendo”
Mgeni Rasmi katika mkutano huu alikua ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ambaye aliwakilishwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Paschal Katambi (Mb) aliyeanza kwa kuwapongeza ATE kwa kuandaa mkutano huu ulioambatana na uchaguzi wa viongozi wake, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti .
Naibu Waziri pia alibainisha kuwa Mjadala wa leo unaonyesha ni kwa kiasi gani ATE) kama mdau wa UTATU inaunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaongezea Vijana Ujuzi ili waweze kuajiriwa na kujiajiri.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran akitoa salamu za ukaribisho alisema kuwa mada ya majadiliano kwa mwaka huu inalenga kuchochea ushiriki wa wadau wa kisekta kwa maana ya Waajiri wote katika sekta kuu za uchumi, wawakilishi wa Vyama vya Wafanyakazi, vyuo mbalimbali vya elimu na ufundi, na serikali kwa ujumla.
Mkutano huu ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Saidi Wamba ambaye aliwashukuru ATE kwa kuwakaribisha katika Mkutano huu na kuahidi kuendeleza ushirikiano miongoni mwao ili kuboresha maslahi ya Waajiri na Wafanyakazi kwa pamoja.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa Ofisi ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda & Burundi, Bw. Jealous Chivore aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Serikali, ATE na TUCTA katika kukuza na kutekeleza sera za kitaifa za ujuzi, mikakati na programu za kukuza ajira, ukuaji wa uchumi na jamii jumuishi.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti Mpya wa ATE, Bw. Oscar Mgaya ambaye alichaguliwa katika Mkutano huu Mkuu wa Wanachama, alimueleza kuwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kinaundwa na Sekta 10 ambapo kila Sekta ina Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambao wanawakilisha Sekta zao katika Bodi ya Wakurugenzi ya ATE na kuahidi kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Viongozi wenzake ili kufikia malengo yaliyokusudiwa