Monday - Friday ( 08:00 AM - 04:30 PM )
ATEATEATE
+255 22 2780023
info@ate.or.tz
Mikocheni Industrial Area, Dar es Salaam

ATE yazindua Mafunzo ya Programu Mwanamke Kiongozi kwa Wajumbe Wanawake wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar

Zanzibar,
17 Februari 2022

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri la Norway (NHO) siku ya  Alhamisi tarehe 17 Februari 2022 wamefanikiwa kuzindua rasmi Mafunzo ya Programu ya Mwanamke Kiongozi kwa Wajumbe Wanawake wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar  ambapo Mgeni Rasmi katika tukio hilo alikuwa ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid aliyewakilishwa na Naibu spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Mgeni Hassan Juma.

Uzinduzi wa Mafunzo haya umefanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Baraza la Wawakilishi Chukwani -Zanzibar na kuhudhuriwa pia na Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elisabeth Jacobsen, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Bi. Leyla Mohammed Mussa aliyemuwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed na Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani kwa Ofisi za Afrika Mashariki Bw. Wellingtone Chibebe. Wengne ni Pamoja na  Viongozi wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar, Wawakilishi wa Wajumbe Wanaume Machampioni wa UWAWAZA, Wajumbe wa Bodi ya ATE, Wataalamu Waelekezi kutoka Chuo cha ESAMI, Wawakilishi kutoka Chama cha Waajiri Zanzibar (ZANEMA).

Mkurugenzi Mtendaji  & Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE)  Bi. Suzanne Ndomba -Doran akitoa salamu za Ukaribisho amesema kuanzishwa kwa mafunzo haya ya Mwanamke Kiongozi kwa Wabunge na Wajumbe Wanawake wa Baraza la Wawakilishi kumetokana na rai aliyotoa Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa Wanawake katika Uongozi ulioandaliwa na ATE, mnamo tarehe 4 Machi 2021 ambapo Mh. Rais alitoa rai kwa ATE kuhakikisha mafunzo haya yanawafikia wanawake wabunge na viongozi wa kisiasa na Sehemu za Umma.

“Kufuatia mapendekezo hayo, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE)  kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri la Norway (NHO) pamoja na Chuo cha Uongozi cha ESAMI tulianza mchakato wa namna ya uwasilishwaji wa Mafunzo haya ikiwemo kuyafanyia marejeo ili Kuhakikisha yanaendana na mahitaji ya Waheshimiwa Wabunge Wanawake na wajumbe wanawake wa Baraza la Wawakilishi. Mafunzo haya yamelenga kuongeza ufanisi wa watakaoyapitia kwenye utekelezaji wa shughuli zao kama Wabunge hususani kama wawakilishi wa wananchi, watunga sheria na sera mbalimbali pamoja na kuisaidia Serikali katika kutimiza majukumu yake ya kila siku” Alisema Bi. Ndomba-Doran.

Bi. Ndomba -Doran aliendelea kwa kusema kwamba Programu hii ya Mwanamke Kiongozi inayosimamiwa  na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri la Norway (NHO) ilianzishwa rasmi nchini mwaka 2016 na kuzinduliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa wakati huo ambaye sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo Mafunzo ya Programu hii yamekuwa yakitolewa katika maeneo makuu Matatu ambayo ni; Uongozi(Leadership), Utawala (Governance) na Uwezo wa Kujenga na kuwasilisha hoja (Rhetoric) na mpaka sasa jumla ya wanawake 201 kutoka katika Taasisi na makampuni 59 wamekwisha patiwa mafunzo haya na kuhitimu. Pia wengi waliopita katika mafunzo haya wamefanikiwa kushika nafasi za juu za uongozi katika Taasisi mbalimbali pamoja na Bodi za wakurugenzi huku mchango wao ukionekana dhahiri.

Akitoa hotuba kwa niaba ya Mgeni Rasmi Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Mgeni Hassan Juma alisema kuwa masomo haya yataenda kuongeza ufanisi na kuwa chachu kwenye maendeleo chanya ya nchi yetu na jambo la muhimu ni kuona mafunzo haya yamezingatia suala la Muungano baada ya kuyazindua katika Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania mmeyaleta na huku kwetu Zanzibar kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

“Nipende kuwahamasisha Waheshimiwa Wajumbe Wanawake kutumia nafasi hii waliyopata vizuri na kuhudhuria mafunzo haya bila kukosa ili waweze kupata matunda yanayotokana na programu hii. Ofisi yangu itatoa ushirikiano kuhakikisha mafunzo haya yanafanikiwa kwa manufaa mapana ya nchi” Alisema Mhe. Naibu spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Mgeni Hassan Juma.