Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) jana Jumatano tarehe 13 Julai 2022 kimeshiriki sherehe za Kufunga Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara Dar es salaam 2022 ambapo Mgeni Rasmi katika tukio hili alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango.
Maonesho ya Mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Tanzania ni Sehemu Sahihi kwa Biashara na Uwekezaji”
ATE imewakilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wake Bi. Suzanne Ndomba-Doran aliyeambatana na Mkuu wa Idara ya Wanachama na Masoko Bi. Patricia Chao sambamba na maafisa wengine kutoka idara ya Miradi na Mawasiliano.
Sherehe za kufunga maonesho hayo yameenda sambamba na Utiaji Saini wa Mikataba mbalimbali ya Kibiashara pamoja na utoaji wa Vyeti na Vikombe kwa washindi wa Maonesho ya mwaka huu.
Tukio hili pia limehudhuriwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (MB), Katibu Mkuu Wizara hiyo Prof. Godius Kahyarara, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Jokate Mwegelo aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omary Said Shaban pamoja na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.