Salamu za waajiri kutoka kwa Bi. Jayne Nyimbo-Taylor

SALAMU ZA WAAJIRI ZILIZOTOLEWA NA BI. JAYNE NYIMBOTAYLOR, MWENYEKITI WA CHAMA CHA WAAJIRI TANZANIA (ATE) KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA WAFANYAKAZI MKOANI MBEYA KATIKA UWANJA WA SOKOINE TAREHE 1 MEI 2019 

Mh. Mgeni Rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, 

Bw. Tumaini Nyamhokya- Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),

Mhe. Jenista Mhagama(Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu,  

Mhe. Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,  

Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wabunge mliopo hapa, 

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya mliopo hapa  

Mheshimiwa Sophia Wambura, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi 

Bw. Wellington Chibebe, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani Ofisi ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi 

Dkt. Aggrey K. Mlimuka-Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE),  

Dkt. Yahya Msigwa-Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), 

Ndugu Waandishi wa Habari, 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, 

Itifaki imezingatiwa!

 

Mei Mosi Oyee...? Wafanyakazi na Waajiri Oyeee….!

Kwa niaba ya waajiri wote wa Tanzania hususani wanachama wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) napenda kutumia fursa hii kuwasalimu wafanyakazi wote wa Tanzania katika siku hii muhimu tunapojumuika na Dunia nzima kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani kwa mwaka huu wa 2019 tunasema hongereni sana!

Waajiri tunapenda kutoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) pamoja na serikali kwa kuendelea kudumisha ushirikiano wetu kama wadau muhimu sana katika mfumo wetu wa Utatu.

Kwa kipekee kabisa niungane na Uongozi wa TUCTA kukushukuru wewe Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwa kukubali kushiriki katika maadhimisho haya ya mwaka huu 2019.

Mh. Mgeni Rasmi, Mabibi na Mabwana,

Tunaipongeza serikali ya awamu ya Tano kwa utendaji wake mahiri hasa katika ujenzi wa Miundombinu ya Kisasa kwani kukamilika kwa miradi hii kutachangia kukua kwa pato la taifa na kuzalisha ajira nyingi na kuharakisha ujenzi wa uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mnamo tarehe 9 Aprili 2019 Mheshimiwa Rais ulipokuwa ziarani mkoani Njombe katika uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata majani ya Chai pamoja na mambo mengine, uliwataka watendaji wa Serikali kupunguza urasimu na vikwazo vyote kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini. Kwa dhati kabisa tunakupongeza Mh. Rais wetu kwa kukemea jambo hili hadharani kwani ili kujenga uchumi wa viwanda ni lazima kama Taifa tutengeneze mazingira rafiki yatakayowavutia wawekezaji wa ndani na nje kwani tusipofanya hivyo suala la kuwa na uchumi wa kati litabaki kuwa ndoto isiyotimia. 

Tungependa Pia kuchukua nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi mzuri wa kuliweka suala la uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kumteua Waziri anayeshughulikia Uwekezaji nchini kwani tunaamini changamoto mbalimbali zinazohusiana na uwekezaji zitatatuliwa kwa karibu na haraka zaidi.

Mh. Mgeni Rasmi, Mabibi na Mabwana

Tunaipongeza serikali kwa kuahidi kupitia na kuzifanyia marekebisho ya sheria za Kazi katika mwaka ujao wa fedha kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa.
Kassim Majaliwa
alivyoahidi wakati wa kuwasilisha hotuba ya Bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka ujao wa fedha Bungeni jijini Dodoma.  Sheia zetu za Kazi za sasa zinalea uzembe, ubadhirifu na wizi mahala pa kazi. Sisi waajiri tungependa kupata ushirikiano wa dhati kutoka kwa wadau wa Utatu katika kufanya marekebisho ya sheria hizi ambayo yatapelekea kuwepo kwa mazingira rafiki ya uwekezaji nchini ambayo yatachochea ukuaji wa haraka wa uchumi wa Taifa letu. 

Mh. Mgeni Rasmi, Mabibi na Mabwana,

Pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanya na serikali yako katika kuhakikisha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini yanakuwa bora, bado waajiri nchini wameendelea kukumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa za kufanya biashara hapa nchini.
Moja ya changamoto hizo ni Tozo Kubwa ya Kuendeleza Ujuzi mahala pa Kazi (SDL) ambapo kwa sasa waajiri wanatozwa asilimia 4.5 Tunaiomba serikali iweze kuipunguza tozo hii kutoka asilimia 4.5 ya sasa mpaka asilimia 2. Gharama nyingine ni pamoja na kodi ya kipato kwa wafanyakazi.

Mh. Mgeni Rasmi, Mabibi na Mabwana,

Kupunguza gharama za uwekezaji na kuboresha mazingira ya uwekezaji yatanufaisha wadau wote na jamii kwa ujumla. Kwa Mwajiri na mwekezaji yanamuongezea faida na kukuza biashara yake. Pia serikali nayo itanufaika kutokana na faida anayopata mwekezaji kupitia kodi ambazo zinaiwezesha serikali kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na huduma za jamii. Wafanyakazi nao watanufaika kwa kupata ajira na kazi zenye staha na kumudu gharama za maisha. Hivyo kwa kuangalia manufaa haya yanayogusa pande zote sisi Waajiri tunapenda kutoa wito kwa Serikali na wadau wote kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kila mmoja kwa nafasi yake aweze kunufaika 

Mh. Mgeni Rasmi, Mabibi na Mabwana,

Naomba nihitimishe salamu zetu kwa kutoa shukrani za pekee kwako Mheshimiwa Rais kwa ushirikiano ambao umekuwa ukiutoa kwa sekta binafsi na dhamira yako ya dhati ya kushughulikia changamoto za kimaendeleo ndani ya nchi yetu.  Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) tupo tayari na tutaaendelea kuipa serikali ushirikiano katika kupeleka mbele gurudumu la maendeleo. 

Nawatakia Maadhimisho mema ya kusherekea siku ya Mei Mosi 2019 na Ahsanteni sana kwa kunisikiliza! 

 

Download the full speech here in PDF.