HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU APRIL 2019

HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU: SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU, MHE. JENISTA JOAKIM MHAGAMA (MB), KATIKA SIKU YA AFYA NA USALAMA MAHALI PA  KAZI DUNIANI – MBEYA TAREHE 28 APRILI 2019.

 • Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb) Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira)
 • Mheshimiwa Stella Alex Ikupa(Mb) Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu)
 • Mheshimiwa William Ntinika Mkuu wa Wilaya ya Mbeya
 • Bw. Andrew Masawe Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)
 • Bw.Tumaini Nyamhokya Rais wa Tucta 
 • Bi Mariam Mtunguja Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya 
 • Dkt Adelehm Meru Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri OSHA 
 • Viongozi wote wa Mkoa wa Mbeya (Mliohudhuria hapa) 
 • Bi Khadija Mwendwa Mtendaji Mkuu OSHA
 • Bwana Dani Sola Mwakilishi wa  Mkurugenzi Mtendaji ATE 
 • Dkt. Yahya Msigwa Katibu Mkuu TUCTA 
 • Mwakilisha wa ILO 
 • Ndugu Viongozi na Watendaji wote mliohudhuria 
 • Waajiri, Wafanyakazi na Wananchi wote
 • Mabibi na Mabwana, na Wageni Waalikwa

Tumsifu Yesu Kristu
Bwaba Asifiwe, 
Assalaam Alaykum.

Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia sote kuwepo hapa leo hii katika maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani, tukiwa wote wazima wa afya njema. Pia napenda kuwashukuru nyote mliohudhuria katika maadhimisho haya kwani inaonesha ni jinsi gani mnavyounga mkono jitihada zinazo chukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya afya na usalama sehemu za kazi. 

Kipekee naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya pamoja na timu yake kwa kukubali kuwa wenyeji wetu ili tuweze kuadhimisha siku hii na ametupatia ushirikiano wa hali ya juu. Niwashukuru pia Viongozi wa Utatu, TUCTA na ATE ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa siku hii ya leo inafanikiwa kama tunavyoona hivi sasa. Niwapongeze pia wenzetu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kuwa siku zote wameendelea kushirikiana na Serikali katika masuala yote yanayohusu kazi na ajira.

Kwa ujumla ninawashukuru waandaaji wa maadhimisho haya wote kwani wao ndo wametuwezesha kukutana hapa leo na pia kwa kunipa nafasi ya kuwa mgeni rasmi na kuzungumza na nanyi katika siku hii muhimu tunapoungana na wenzetu duniani kote. 

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana

Kama ilivyo kawaida ya kila mwaka, tunapoadhimisha siku hii tunafuata kauli mbiu inayotumika Duniani kote ambayo hutolewa na Shirika la Kazi la Dunia. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Usalama na Afya na Mstakabali wa Kazi – Safety and Heath and the future of work ”.  Lakini kulingana na mazingira ya Nchi yetu kwa sasa ambapo tunajenga uchumi wa viwanda, nasi tumetengeneza kauli mbiu yetu ili kuendana na mazingira tuliyonayo, ambapo kauli mbiu hiyo imeboreshwa na imekuwa ni “Usalama na Afya na Mstakabali wa Kazi kuelekea Uchumi wa Viwanda – Safety and Heath and the future of work towards Industrial Econmy”

Hii inatwambia kwamba suala la usalama na afya mahali pa kazi litakuwa ndio kiini cha mustakabali wa kazi hasa wakati nchi yetu inaendelea kujenga uchumi wa viwanda na kuelekea uchumi wa kati. Kukua kwa haraka kwa teknolojia inayotumika katika viwanda na maeneo mengine ya  kazi kunagusa moja kwa moja afya na usalama ya wafanyakazi. Kuongezeka kwa vifaa vya digitali na matumizi ya teknolojia kumebadilisha kabisa mazingira ya kazi hususan kuongezeka kwa vihatarishi vipya mahali pa kazi

Uchafuzi  wa  mazingira kutokana na baadhi ya shughuli za uzalishaji Viwandani, Migodini na baadhi ya shughuli nyingine za binadamu umesababisha mabadiliko ya tabia nchi. Mabadiliko hayo ni kama vile kuongezeka kwa joto duniani, mvua kutonyesha kwa wakati na pengine kutonyesha kabisa au kunyesha kupita kiasi. Mabadiliko hayo tunayashuhudia hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Mabadiliko ya tabia nchi ni moja katika mambo makubwa yanayochangia mustakabali wa kazi. Uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za kiuchumi mfano uchimbaji wa madini na shughuli za viwandani unaleta athari za moja kwa moja katika afya za wafanyakazi pamoja na umma kwa ujumla. Katika juhudi za kupambana na hali hiyo kwa sasa Duniani kote msisitizo umekuwa ni kuhamasisha kazi kijani (green jobs) na viwanda vinahimizwa kupunguza hewa ukaa hali ambayo itasaidia kupunguza vihatarishi sehemu za kazi na hatimaye kupunguza madhara ya kiafya kwa wafanyakazi.

Ndugu Wageni Waalikwa Mabibi na mbwana 

Mahitaji ya dunia yanayotokana na utandawazi yamepelekea kuwepo na idadi kubwa ya wafanyakazi wanaofanya kazi masaa mengi kuliko kawaida na aina nyingine za ajira ambazo hazina viwango na zenye vihatarishi vingi. Kwa sababu hiyo imekuwa ni muhimu sana kwa sasa kuliko wakati wowote kuanza kutambua vihatarishi vipya katika maeneo ya kazi. Kutambua vihatarishi hivyo ni hatua muhimu ya kwanza kabisa itakayopelekea kuweka mikakati ya kuzuia vihatarishi hivyo ili wafanyakazi wasipate ajali na magojwa yatokanayo na kazi. Ajali na magonjwa yatokanayo na kazi ni mambo ambayo yanaweza kuzuilika kwa kuwa vyanzo vyake vinaweza kutambulika na kuonekana tangu mapema kama tutakuwa makini. Ili kutambua vyanzo hivyo ni muhimu tukajenga utamaduni wa masuala ya afya na usalama mahali pa kazi miongoni mwa jamii. Katika kujenga utamaduni wa kuzuia vihatarishi sehemu za kazi ni wakati muafaka sasa kwa nchi yetu kuingiza masuala ya afya na usalama kazini katika mitaala ya elimu yetu mfano vyuo vya veta na vyuo vyote vya ufundi. Hali hiyo itakayowawezesha wahitimu kupata ufahamu wa masuala hayo kabla hata hawajaingia kwenye soko la ajira na hatimaye kuiwezesha nchi kuwa na wafanya kazi wa baadae wenye afya na walioko salama.

Ni vizuri kutambua kuwa suala la afya na usalama kazi sio tu ni suala la kisheria bali ni suala la wajibu wa kimaadili, ni wajibu kwa jamii na linachangia katika ukuzaji wa biashara. Tafiti zinaonyesha kuwa kila shilingi moja inayowekezwa kwenye masuala ya afya na usalama kazini huleta faida ya zaidi ya shilingi mbili

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Kuwekeza kwenye afya na usalama kazini kunaleta faida nyingi. Baadhi ya faida hizo ni pamoja na kuzuia madhara kwa wafanyakazi na kulinda nguvukazi muhimu ya Taifa letu, kunaleta hamasa na ari ya kufanya kazi kwa bidii miongoni mwa wafanyakazi, kuimarisha mahusiano mazuri na jamii, kuongeza ubora wa bidhaa au huduma inayotolewa na kampuni husika, n.k

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Katika kuboresha mazingira ya biashara Nchini tumeendelea kusimamia suala Usalama na Afya mahala pa kazi ikiwa ni pamoja na  kusisitiza kupunguza gharama na kuondoa urasimu katika kutoa huduma kwa wawekezji kwa kupunguza tozo na ada mbalimbali jambo hili limetekelezwa  kama ifuatavyo; 
Kuondoa Ada na Tozo mbalimbali tano ambazo ni 

 1. Kuondoa Ada ya Usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya Sh. 50,000 hadi Sh.1, 800,000; 
 2. Kuondoa Ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi iliyokuwa ikitozwa Sh. 2,000; 
 3. Kufuta Faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto ya Sh. 500,000; 
 4. Kuondoa Ada ya Leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama iliyokuwa inatozwa Sh 200,000 kwa mwaka; na
 5. Kuondoa Tozo ya Ushauri wa kitaalamu wa Usalama na Afya ya Sh 450,000 kwa saa

Kutokana na mabadiliko haya kumekuwa na ongezeko la usajili wa sehemu za kazi toka 2,845 mwaka 2015 hadi 8,392 mwaka 2018. Pia Elimu kwa wenye Viwanda vidogo na Wajasiriamali na Vikundi vya walemavu wanaojishughulisha na usindikaji wa vyakula, Ushonaji na utengenezaji Batiki wapatao 16,897  wamepewa elimu ya kugundua vihatarishi. 

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Kuimarisha afya na usalama kazini sio lazima iwe ni kuongeza matumizi ya fedha. Kitu cha msingi ni kuhakikisha kuwa viongozi mahali pa kazi wanakuwa mstari wa mbele katika kuzuia ajali sehemu za kazi na kutengeneza mazingira ya kuaminika na kuwasiliana kwa uwazi katika ngazi zote. 

Mabadiliko ya kazi yanatokea tukiwa tunashuhudia na yanaleta fursa za aina yake katika ustawi wa jamii na wakati huo huo yanaleta changamoto mpya. Imekuwa pia ni vigumu kutabili ni aina gani mpya ya teknolojia itakuja na ni namna gani itatumiwa sehemu za kazi na itaweza kuleta madhara gani kwa wafanyakazi. Kwa hiyo tunapaswa kuweka mikakati imara ya kupambana na hali hiyo ambayo hatuijui kwa kujenga uwezo wa kitaaluma miongoni mwa Watalaam wetu na kujenga uwezo wa kufanya tafiti za kisayansi ili tuwe tayari kupambana na hali yoyote itakayojitokeze huko mbele. Kazi iliyoko mbele ni kubwa hivyo tunawaomba Waajiri, Wafayakazi na umma kwa ujumla kushirikiana na Serikali ili tuweze kuimarisha afya na usalama kazini na mstakabali wa kazi. Huu ndio wakati wa kuchukua hatua.

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Ndugu wadau bado tuna changamoto kubwa ya ajira mbaya kwa watoto wetu. Watoto wengi wanaajiriwa katika migodi, mashambani na sehemu nyingine ambazo watoto hawapaswi kufanya kazi. Jambo baya zaidi ni kuwa watoto hao wanaacha kwenda shule. Matokeo ya utafiti wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali uliochapishwa mwaka 2016 inaonyesha kuwa watoto wenye umri kati miaka 5 – 17 walioko kwenye ajira ni takribani milioni 4.2 ambayo ni asilimia 28.8 ya wafanyakazi wote. Na katika hao asilimia 21.5 wako kwenye ajira hatarishi. Hali ni mbaya zaidi katika sehemu za mashambani ambako asilimia 35.6 ya wafanyakazi wote ni watoto. Watoto wengine wanajishughulisha na kazi katika sekta za madini, misitu na uvuvi. Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa asilimia 11.1 (468,392) ya watoto walioko kwenye ajira, walipata ajali au magonjwa yatokanayo na kazi na wengine hata kupoteza maisha. Takwimu hizo zinatwambia kwamba, nguvu kazi ya baadaye tunayotegemea katika kuzalisha na kuendesha uchumi wa viwanada itapata pigo kubwa hali itakayopelekea tusifikie lengo letu la uchumi wa kati ifikapo 2025.

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Zipo changamoto nyingi zinawaweka vijana katika hali hatarishi wanapokuwa sehemu za kazi. Changamoto hizo ni kama vile hatua walioko ya ukuaji wa kimwili na kisaikolojia hali inayowafanya wao kuwa rahisi kudhurika na vihatarishi wakiwa kazini, ukosefu wa uzoefu kazini, ukosefu wa mafunzo na stadi za kazi, kutokuwa na ufahamu wa kutosha juu vihatarishi katika sehemu zao za kazi pamoja na kukosa nguvu ya majadiliano kazini ambayo inapelekea kukubali kuajiriwa katika kazi hatarishi au katika kazi zenye mazingira mabaya ya kazi.

Kutokana na ukosefu wa ajira, vijana wetu wengi wanajikuta wanaajiriwa katika kazi hatarishi jamabo ambalo linaweza kufanya afya na usalama wao kuwa hatarini. Kwa hiyo ili kuzuia ajira hatarishi ni lazima waajiri wahakikishe kazi iwe yenye staha kwa kuwa na sifa zifuatazo: kazi salama yenye hadhi, inayolinda  heshima na utu wa kijana, yenye kuleta kipato stahili, inayoleta amani sehemu za kazi,  na yenye kukuza uchumi na kuongeza tija na pato la vijana na Nchi kwa ujumla.  Na ili kazi iwe na sifa hizo ni lazima kudhibiti hali zote hatarishi zinazoweza kufanya mazingira ya kazi yasiwe salama. 

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Sekta isiyo rasmi ni sekta muhimu sana na ina mchango mkubwa katika uchumi na maendeleo ya Nchi yetu. Sekta isiyorasmi inaajiri vijana wengi hapa Nchini, japokuwa sekta hii bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Ukiachilia mbali changamoto za mitaji, pia suala zima la afya na usalama mahali pa kazi. Wajasiliamali hao hawana rasilimali fedha kugharimia huduma za afya na usalama kazini, ufahamu mdogo wa vihatarishi kazini, na ukosefu wa vifaa kinga, hali inayopelekea kutokea kwa ajali na magojwa yatokanayo na kazi. Kwa maana hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine tunatoa elimu kwa wajasiliamali hao ili waweze kutambua na kuzuia vihatarishi vilivyopo katika mazingira yao. Nimeelezwa kuwa kabla ya siku ya kilele cha  maadhimisho ya siku ya leo wajasiliamali toka sekta mbalimbali katika mikoa ya Njombe, Songwe na Mbeya wapatao 1,600 wamepata mafunzo. Naomba kuwapongeza sana waliojitokeza kupata mafunzo haya.

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inashughulika pia na masuala ya UKIMWI  Mahala pa Kazi na UKIMWI kwa ujumla , naomba niongelee Janga la ukimwi na virusi vya UKIMWI linendela kuwa changamoto kubwa katika Nchi yetu. Kwa maana hiyo ni lazima tuendelea kukumbushana kwamba suala la janga la UKIMWI lina mchango mkubwa katika mstakabali wa kazi na suala hili linagusha wafanayakazi moja kwa moja kwa kuwa ndio walioko kwenye umri hatarishi. Janga hili linaathiri zaidi nguvu kazi inayotegemewa na Nchi hasa Vijana. Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/17 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) inaonyesha kuwa maambukizi kwa Watanznia ni asilimia 5% tayari wameambukizwa na kati yao wanawake ni asilimia 6.3% na Wanaume 3.4% Mkoa wa Mbeya maambukizi yako juu imefikia asilimia 9.3%, wanaoongoza ni Mkoa wa Njombe 11.4% wakifuatiwa na Iringa 11.3%, Songwe 5.8% na Ruvuma 5.6% unaweza ukaona Kanda ya Nyanda za Juu hali ilivyo mbaya sana. 
Kwa Mujibu wa Utafiti wa Nguvu kati uliofanyika Mwaka 2014  ulibainisha kuwa asilima 56% ya Nguvu kazi ni Vijana na kwa mujibu wa utafiti wa UKIMWI kila mwaka vijana 28,000 wenye umri kati ya miaka 15-24 hupata maambukizi mapya na  asilimia 80% ya maambukizi mapya kwa vijana ni watoto wa kike hivyo unaweza kuona ni namna gani nguvu kazi ya Taifa ilivyo hatarini. 
Aidha Takwimu zinaonesha kuwa Watu wengi bado hawajitokezi kupima na hasa wanaume, hivyo naomba nitoe wito kwa wanaume kujitokeza kwa wingi kupima na ikigundulika kuwa umeathirika unaanza dawa mara moja . Lengo latu ni kuwa ifikapo 2020 asilimia 90% wawe wanajua hali zao, asilimia 90% wawe wameanza kutumia dawa na asilimia 90% wawe wemefubaza virusi vya UKIMWI. UKIMWI hauna dawa lakini ukijua hali yako ukaanza kutumia dawa maisha yako ynaendelea kama kawaida.

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Aidha niwaombe  wadau, wote tushirikiane kutoa elimu katika maeneo yetu ya kazi ili kupunguza au kuzuia kabisa maambukizi mapya sehemu za kazi, kuondoa unyanyapaa na ubaguzi, na kujaribu kuwasaidia wale wafanyakazi ambao tayari wameathirika kwa kuwapatia uwezo wa kupata lishe bora na ikiwezekana kuwawezesha kupata matibabu ya magonjwa nyemelezi kila yanopojitokeza.

Ndugu wageni waalikwa Mabibi na Mabwana 

Mwisho naomba kuwashukuru kwa ushiriki wenu na pia mtambue kuwa Serikali  imeendela kuthamini juhudi za makampuni binafsi,  Taasisi za Umma kwa kushirikiana na wafanyakazi wanaojituma katika kuboresha  mazingira ya kazi kwa mujibu wa Sheria na Waajiri wote wanaofanya ubunifu wa kuboresha mazingira ya kazi wao wenyewe bila kusukumwa. Hivyo kwa kupitia Wakala wa Usalama na Afya mahali pa Kazi (OSHA), Serikali imeanzisha tuzo maalumu kwa Taasisi zinazoonesha juhudi katika kuboresha mazingira ya kazi na kuweka mifumo ya afya na usalama kazini iliyoimara na inayoleta tija katika sehemu za kazi. Hivyo napenda kuchukua fursa hii kuzipongeza kampuni zilizofanikiwa kupata tuzo mwaka huu. 

Nimalizie kwa kusisitiza kuwa, Serikali ya awamu ya tano itaendelea kuhamasisha suala la usalama na afya mahala pa kazi hasa wakati huu tunapojenga uchumi wa viwanda ambao kwa hakika unaambata na na vihatarishi  vipya. Tutaendelea kushirikiana na wadau kupunguza au kuondoa kabisa vifo, ajali, magonjwa na madhara yatokanayo na kazi. 

Baada ya kusema hayo napenda kuwashukuru wote mlioshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya na ninawatakia mchana mwema. 

Asante kwa kunisikiliza. 

 

Download the full speech here in PDF.