Hotuba iliyosomwa na DKT. Aggrey Mlimuka

HOTUBA ILIYOSOMWA NA DKT. AGGREY MLIMUKA, MKURUGENZI MTENDAJI WA CHAMA CHA WAAJIRI TANZANIA (ATE) SIKU YA UZINDUZI WA TUZO YA MWAJIRI BORA WA MWAKA 2019, JUMATATU TAREHE 29 APRIL 2019, DAR ES SALAAM.

Ndugu Waandishi wa Habari, 
 
Timu ya EYA 2019 na Mshauri wetu Mwelekezi, 
 
Mabibi na Mabwana, 
 
Habari za Asubuhi!

Awali ya yote napenda kuwashukuru kwa kuja kujumuika na sisi asubuhi hii katika tukio hili muhimu sana katika kalenda ya Chama chetu. Lengo kuu la kukutana hapa ni kuwafamisha kuwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) leo tunazindua rasmi Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka 2019 ambayo pamoja na mambo mengine ni kutaka kutambua na kutoa tuzo kwa Waajiri wenye misingi bora ya usimamizi wa nguvu kazi na rasilimali watu ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kibiashara. Tuzo hizi mwaka huu pia zimepanuka sio tu kujali rasilimali watu bali pia kutambua Waajiri wanaofuta taratibu za kitaifa na kimataifa katika uendeshaji wa biashara zao. 

Zoezi hili linalenga kutambua mchango wa rasilimali watu ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kibiashara. Tuzo ya mwajiri bora wa mwaka (EYA) ni zoezi lililoanzishwa na kuendeshwa kila mwaka na Chama cha Waajiri Tanzania tangu mwaka 2005.

Tuzo ya mwajiri bora wa mwaka inalenga zaidi kuwatambua wanachama waliofanya vizuri katika kuweka mikakati bora yenye kuthamini usimamizi wa rasilimali watu na shughuli za kibiashara. Kwa miaka kadhaa tuzo hizi zimehamasisha makampuni wanachama kuweka juhudi katika masuala ya ajira na usimamizi wa rasilimali watu kama msingi mkakati wa makampuni yao kujenga nguvu kazi yenye ujuzi,furaha, ushindani, na yenye kushiriki kikamilifu katika uzalishaji.

Kutokana na maoni tuliyopokea kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wadau na wataalamu wetu mbalimbali, tuzo ya mwajiri bora kwa mwaka huu 2019 imekuja na vipengele vipya vitatu (3) na kufanya kuwa na Jumla ya vipele 38 kutoka vipengele 35 tulivyokuwa navyo mwaka jana. Vipengele vilivyoongezeka ni 

  • Mwajiri Bora anaeendaleza Mafunzo ya Ujuzi wa Kazi kwa wahitimu (Internship) 
  • Mwajiri Bora anayetoa mafunzo ya Uanagenzi (Apprentiship)
  • Mwajiri Bora anayezingatia Haki Rasilimali ijulikanavyo kama Local Content 

Lengo la kuongeza vipengele hivi ni kuendelea kuziboresha tuzo hii na kuongeza ushindani miongoni mwa washiriki na pia kujaribu kugusa kila eneo ambalo litaleta tija katika ukuzaji na uendelezaji wa rasilimali watu katika maeneo ya kazi.

Tuzo hizo mpya zitakuwa ni nyongeza ya zile ambazo zimekuwa zikitolewa katika  masuala ya utawala na uongozi, ubora katika usimamizi wa rasilimali watu, bidhaa au huduma, uzalishaji na ubunifu, uwajibikaji katika mwenendo wa biashara, utendaji unaokidhi, ushirikishwaji wa mwajiriwa, ukuzaji wa vipaji, mafunzo na maendeleo pamoja na usalama wa mwajiriwa katika mazingira ya kazi. Tuzo nyingine ni ile  ya uwiano wa kazi na maisha,  mwajiri bora ni yule anayesimamia vema nguvu kazi inayoonekana kupotea/kupuuzwa, Waajiri bora wenye mikakati inayojali afya za waajiriwa, tuzo ya utofautishwaji na ushirikishwaji yaani (diversity and inclusion), Waajiri bora waonaowachochea na kuwajali waajiriwa wenye ujuzi, Waajiri bora wenye mahusiano mazuri baina ya waajiri na waajiriwa, Waajiri bora wenye majina makubwa na imara huvutia wateja, waajiriwa, wadau na mwajiri bora aliyewekeza kwenye teknolojia.

Pia tutaendelea kuwa na Tuzo ya Mshindi wa Jumla (Overall) na tuzo kulingana na ukubwa, nazo ni zile zinazohisu tuzo ya waajiri bora katika sekta binafsi, sekta za umma pamoja na mashirika ya ndani ya nchi.

Ushiriki wa Tuzo ya Mwajiri Bora umeendelea kuongezeka kutokana na ukweli kuwa waajiri wengi wamehamasishwa kuthamini watu katika kufanikisha shughuli za biashara kama nyanja muhimu ya usimamizi wa rasilimali watu mahali pa kazi.

Pia nipende kutumia fursa hii kuwafahamisha kwamba kitabu cha Mwongozo wa Misingi Muhimu ya Kusimamia Rasilimali Watu ya Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka kipo tayari hivyo niwaombe waajiri wote waweze kujipatia mwongozo huu utakaoelekeza makampuni mambo ya kuzingatia katika usimamizi wa rasilimali watu ili kuongeza tija na kuongeza ushindani. Kimsingi, mwongozo huu tulioouandaa utakuwa na madhumuni yafuatayo:

  • Kushawishi, kuelimisha na kusaidia wanachama wa ATE juu ya umuhimu wa rasilimali watu, mifumo na stadi zinazohitajika ili kujenga taasisi imara, 
  • Kuelekeza makampuni namna ya kufuata misingi bora ya rasilimali watu, mifumo na stadi. Viwango hivyo vya kuzingatia vimeanzishwa ili kumwezesha mwajiri kutengeneza sera za kusimamia rasilimali watu, mifumo na stadi. Makampuni yatatumia viwango hivyo katika kupima misingi ya rasilimali watu, mifumo na stadi na kuamua kuboresha misingi hiyo kwa kufuata viwango vilivyotajwa katika miongozo.
  • Kutoa mwongozo kwa ATE katika kusaidia wanachama wake na wengine katika kuboresha usimamizi wa Rasilimali watu, mifumo na stadi. Kimsingi mashirika mengi yanatafuta rasilimali na msaada ili kutimiza wajibu wao wa kusimamia rasilimali watu 
  • Kutoa msaada kwa wanachama wa ATE katika kujiandaa na kushiriki katika Tuzo ya Mwajiri Bora kwa kujiamini na kwa ufanisi.

Kama ilivyoada Shughuli hii ina sehemu mbili; sehemu ya kwanza ni ya utafitiitakayopelekea kupata washindi na kwa sasa sehemu hiyo ipo chini ya kampuni binafsi, TanzConsult inayoongozwa na Prof. BAT Kundi, na sehemu ya pili ni usimamizi wa matukio mpaka kilele cha sherehe ambacho kimepangwa kufanyika mapema mwezi Desemba 2019.

Hivi wanachama waajiri watatarifiwa kutembelea tovuti maalumu kwa tuzo hizi www.eya.co.tz kwa ajili ya kujua Zaidi jinsi ya kushiki. Mwaka huu pia tumeamua kuanza mchakato huu mapema Zaidi ili kuwapa Waajiri wengi muda wa kujiandaa.

Nawasihi wanachama wote kushiriki mashindano haya ili kupata fursa ya kulinganisha utendaji wa makampuni yao na ya wengine. 

Ahsanteni kwa kunisikiliza!

 

Download the full speech here in PDF.