ATE YAFANYA MKUTANO MKUU WA KWANZA WA WANAWAKE KATIKA UONGOZI KWA MWAKA 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

ATE YAFANYA   MKUTANO MKUU WA KWANZA WA WANAWAKE KATIKA UONGOZI KWA MWAKA 2018

 

Dar es Salaam, Jumatatu, 19 Novemba 2018

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri Nchini Norway (Confederation of Norwegian Enterprise, NHO)  Jumatatu tarehe 19 Novemba 2018 Jijini Dar es salaam  wamefanya  Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Wanawake Katika Uongozi kwa Mwaka 2018 ulioambatana na Mahafali ya Pili ya Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao (Female Future Programme)  yenye lengo la kuwajengea uwezo wanawake kwa ajili ya kushika nafasi za juu za uongozi na kuwapa uwezo wa kuingia kwenye Bodi mbalimbali na kushiriki katika kutoa maamuzi .

 

Akifungua Mkutano huo Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge , Kazi , Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista Mhagama (MB)   alisema  Mkutano huu Mkubwa wa Mwaka wa Uongozi kwa Wanawake  unaenda sambamba kabisa na juhudi za nchi yetu kuhakikisha idadi ya wanawake katika nafasi za juu za uongozi inazidi kuongezeka pia wanawake kuwa na idadi kubwa ya uwakilishi katika Bodi za Wakurugenzi za makampuni mbalimbali.

 

“Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea kusimamia kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa viongozi wanawake ndani ya Serikali na Jumuiya mbalimbali na makampuni ya kibiashara nchini na katika kufanikisha hili Serikali yetu imeanzisha Mpango Mkakati wa Kitaifa kwaajili ya Maendeleo ya Usawa wa kijinsia ambao upo kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 ambapo serikali imejizatiti kuunga mkono mpango huu kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia katika shughuli za kiuchumi, Elimu, Mafunzo mbalimbali na Ajira katika Nyanja zote” Alisema Waziri Mhagama.

 

“Programu hii kwangu ni fursa kwenu na mafunzo haya mkiyatumia vizuri yatawasaidia kuendesha maisha katika Nyanja mbali mbali: kazini, nyumbani, kwenye jamii na kwa kizazi chetu kijacho” aliongeza Mh. Waziri Mhagama

 Naye Mkurugenzi wa ATE, Dkt. Aggrey Mlimuka alisema kuwa katika Awamu ya Pili ya Programu ya Mwanamke wa Wakati ujao ATE wameweza kutoa mafunzo kwa Wanawake 25 kutoka kampuni na Taasisi 16.

“Tumetoa mafunzo haya kwa kushirikiana na Chuo cha Mafunzo ya Uongozi Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI) na katika awamu hii ya Pili ya mafunzo jumla ya wanawake 25 kutoka katika makampuni na Taasisi 16 ambayo yamefadhili mafunzo haya yaliyokuwa na sehemu kuu tatu ambazo ni Uongozi, Ufanisi katika Bodi na Ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mahali pa Kazi”

Dkt. Mlimuka alizitaja kampuni zilizoshiriki mafunzo hayo kuwa ni

 • HJFMRI
 • NMB Bank PLC
 • PSSSF Pension Fund
 • Danish Embassy
 • e-Government
 • Geita Gold Mining
 • EFC
 • Songas Gas Ltd
 • Equinor
 • TPB Bank Plc
 • CCBRT
 • ACACIA
 • National Housing Corporation (NHC),
 • Standard Chartered Bank
 • Alistair
   

Dkt. Mlimuka aliongeza kuwa Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao imelenga hasa kujenga uwezo Wanawake katika kuongoza kwenye Nafasi za juu na kuleta matokeo makubwa katika kampuni na taasisi zao pasipo kuathiri majukumu yao Binafsi.

 

“Programu ya Mwanamke wa Wakati ujao ina Malengo Makuu matatu ambayo ni Kupata Wanawake wengi Zaidi kwenye nafasi za juu za uongozi, kwenye hatua za kufanya maamuzi na pia kwenye Bodi Mbalimbali za Wakurugenzi, Pili ni kuwahamasisha na kuwapa changamoto viongozi wanawake kufanya kazi kwa juhudi na malengo makubwa ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya kwenye makampuni na taasisi zao wanazoziongoza na Tatu ni Kutengeneza Jukwaa kubwa la Wanawake kwa ngazi zote kuka pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusiana na uongozi” Alifafanua Dr. Mlimuka

 

Akitoa salamu zake Mwenyekiti wa ATE Bi. Jayne Nyimbo alisema kuwa Mkutano huu Mkuu wa Uongozi kwa Wanawake uliobeba kauli mbiu ya wenye kauli mbiu isemayo “Uongozi wenye Ufanisi kwa Mazingira yanayobadilika Kibiashara” ni moja ya mkakati wa Programu ya Mwanamke wa wakati ujao wa kuhakikisha inawaleta pamoja wanawake na kuwawezesha kukua kiuongozi.

“ATE tukiwa ndio wawakilishi wa waajiri wote nchini furaha yetu ni kuona wanachama wetu ambao ni taasisi na makampuni mbalimbali wanakuwa na Viongozi wanawake wenye uwezo mkubwa lengo likiwa kuongeza uzalishaji wa taasisi zao na taifa kwa ujumla” Alisema Bi. Nyimbo.

 

Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Wanawake Katika Uongozi kwa Mwaka 2018 ulioambatana na Mahafali ya Pili ya Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao (Female Future Programme) Umehudhuriwa na watu mbalimbali kama vile Viongozi wa Serikali, Wakurugenzi wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi, Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali.

 

KUHUSU PROGRAMU YA MWANAMKE WA WAKATI UJAO /FEMALE FUTURE PROGRAMME

Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao ni maalumu kwa Mwanamke wa Afrika kuweza kuhimili nafasi za uongozi katika bodi, biashara, siasa kitaifa na kimataifa. Ni programu maalumu na ya kipekee Afrika iliyotengenezwa kwa lengo la kuhamasisha usawa wa jinsia katika uchumi, elimu na ajira bora.  Kwa kifupi, programu hii humuhamasisha mwanamke kushika nafasi za juu za uongozi.

Programu hii ya mwanamke wa wakati ujao hutoa mafunzo juu ya Uongozi, Ufanisi katika bodi na Ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mahali pa kazi na katika maisha yao kwa kushirikiana na ESAMI kwa muda wa miezi tisa ambapo kutakuwa na muda wa darasani wa siku 14 kwa kozi zote tatu. Mafunzo hayo hutolewa kwa njia mbali mbali zikiwemo midahalo, majadiliano na majaribio na hutolewa kwa kuunganishwa na shughuli za kila siku za muhusika mahali pake pa kazi.

 Programu kama hii ilianzishwa nchini Norway miaka kumi iliyopita na Shirikisho la vyama vya Waajiri (NHO) na ilifanikiwa sana kuongeza wanawake viongozi nchini humo, Uganda, Kenya na sasa ikaletwa Tanzanzani mwaka 2016 na kuzinduliwa na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu na mpaka sasa jumla ya wanawake 66 wamepatiwa mafunzo haya ambapo awamu ya kwanza walikuwa 36 kwa mwaka 2016 na awamu ya 2 walikuwa 30 kwa mwaka 2017 na hadi tunavyozungumza sasa tupo kwenye Awamu ya 3 na jumla ya Wanawake 20 wanaendelea kupatiwa mafunzo haya.

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE)

SLP 2971

DAR ES SALAAM

0764978162/0657453618

kanuda@ate.or.tz